Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari yaliyofanyika tarehe 11/05/2015 kuhusu Kiswahili, Mzee Ali Hassan Mwinyi alisema kuwa inaaminika kuwa Kiswahili ni lugha ya asili ya Afrika. Hii ni lugha inayozungumzwa na watu wengi zaidi kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alieleza kuwa hii ni lugha ya taifa kwa nchi za Kenya na Tanzania. Pia inazungumzwa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda na Visiwa vya Comoro.
Alisisitiza kuwa takriban watu wapatao 100 milioni wanazungumza Kiswahili na ndio lugha pekee ya Kiafrika miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika shughuli rasmi za Umoja wa Afrika.
Matumizi ya Kiswahili yako katika kutoa habari kwa kutumia vyombo vya mawasiliano kama redio, rununga, magazeti na majarida mbalimbali. Alisema kuwa Kiswahili hutumika kama lugha ya kufundishia na kujifunzia katika shule, vyuo, kwenye shughuli za kiofisi, kidiplomasia na hata kwa masuala ya usalama miongoni mwa mataifa. Hata hivyo, licha ya ukubwa wake Kiswahili kinakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Hivi karibuni Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kilifanya mkutano wake wanne ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Ali Hassan Mwinyi.
Rais Mwinyi amekuwa mkarimu sana kuhudhuria hafla mbalimbali za Kiswahili na leo amekubali kuzungumzia Kiswahili na changamoto zake.