CULTURE

Jifunze Kiswahili uwafunze na wengine


HATUTAKIWI tuwe wachoyo tunapojifunza lugha. Kile tunachofahamu tuwamegee na wengine ili kuwasaidia kuwa bora zaidi. Labda yafaa nitoe mfano uliotokea hivi karibuni huko Uingereza.

Wabunge wa Bunge la Uingereza ambao ni weledi wa lugha ya Kiingereza hawaridhishwi na jinsi lugha hii inavyofundishwa. Wameshauri kuwa vyuo vya lugha vipatiwe fedha zaidi katika bajeti kila mwaka. Pamoja na kutilia mkazo mafunzo ya lugha yao wamesisitiza pia lugha za kigeni zisomeshwe hasa kwa wanadiplomasia.

Kamati ya Nje ya Bunge wameshauri kuwa kupandishwa vyeo kwa watumishi wa serikali kutokane pia na kujua Kiingereza barabara na pia mojawapo ya lugha za kigeni. Bajeti kwa mafunzo ya lugha imeongezeka kutoka $ 3 milioni kwa mwaka 2011/12 hadi $ 3.9 milioni kwa mwaka 2013/14. Idadi ya wanafunzi wa lugha kwa mwaka ni 1000. Lugha ya Mandarin ambayo ni lugha rasmi na lugha ya taifa la Wachina ilipendekezwa kufundishwa. Lugha nyingine zinazotiliwa mkazo ni Kihispania na Kireno. Lugha hizi zinatumika nchi za Amerika ya Kusini (Amerika ya Latino) kama Brazil, Cuba, Venezuela, n.k. (Kireno) na Argentina, Chile, Urugauay, n.k. (Kihispsnia). Lugha ya Kiarabu nayo inatiliwa mkazo kama lugha muhimu kwao.

Je, Waingereza wamegundua nini walipoamua kufungua tena chuo chao cha lugha walichofunga mwaka 2007 ? Bila shaka wamegundua kuwa nafasi ya lugha ni kubwa duniani hasa katika diplomasia, biashara, siasa na uchumi. Uamuzi wa kujifunza lugha ya Mandarin, Kihispania na Kireno ni kuwawezesha Waingereza kujua kwa undani masuala mengi yanayowahusu Wachina, wa Amerika ya Kusini na Waarabu katika biashara. Kwa upande wa Kiarabu ni dhahiri kuwa hili ni suala la mafuta.

Katika bara la Afrika, ziko lugha tofauti ambazo zinatufanya tusielewane kutokana na sababu za kihistoria. Nchi za Afrika zinatumia lugha zenye asili ya kikoloni kama Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kiingereza. Hizi ndizo lugha zinazotumika katika vikao vya Umoja wa Afrika (AU).

Lugha ya Kiafrika iliyokubaliwa kutumika ni Kiswahili na Tanzania ilipewa jukumu la kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili kifikie hadhi ya Kimataifa.Tumefika wapi tangu mwaka 1988 tulipoteuliwa na Kikao cha Mawaziri wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) kuwa ni mratibu wa mafunzo ya ukalimani na tafsiri kwa ajili ya kazi za Umoja wa Nchi Huru za Afrika?

Ifahamike kuwa mipango ya ndani ya ukuzaji lugha imekwama kutokana na kutokuwepo sera ya lugha iliyo wazi. Kila waziri mwenye wadhifa wa kusimamia lugha anapoteuliwa huwa na mawazo yasiyotupeleka mbali katika kukifanya Kiswahili kiwe ni lugha ya kimataifa.

Kilikuwapo chuo cha lugha huko Zanzibar lilichojulikana kama Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI). Chuo hiki ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Serikali (SUZA). Chuo hiki kilikuwa na kila sababu ya kuitwa Chuo cha Lugha kwani baadhi ya wanafunzi wake ni wahadhiri wako nchi za nje wakifundisha Kiswahili katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani, Uingereza, China, India na Japan na wengine wana nyadhifa za juu serikalini na katika Bunge letu na baadhi yao wako katika Chama cha Mapinduzi chenye mamlaka ya juu hapa nchini.

Imetamkwa kijumlajumla katika Sera ya Elimu na Mafuzo ya mwaka 2014 kuwa Kiswahili kitaimarishwa katika shule zetu na pia katika Katiba Inayopendekezwa, Kiswahili kimependekezwa kuwa ni Tunu ya Taifa.

TO BE CONTINUED………NEXT WEEK