Mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada ya kibinadam, yameonya kuwa huenda yakalazimika kusitisha shughuli zao zote nchini Somalia, ikiwa Kenya itabadili uamuzi wake wa kufunga vituo vya kutuma na kubadilisha sarafu za kigeni maarufu kama hawala, kufuatia shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Al shabaab, katika chuo kimoja kikuu mjini Garissa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashirika kumi na tano ya misaada, mashirika hayo hutumia vituo hivyo kutuma pesa nchini Somalia na kulipa mishahara na kodi kwa wafanyakazi wake.
Mashirika hayo yamesema, agizo hilo litakuwa na athari kubwa sana kwa raia masikini wa Somalia, kwa sababu wao hutegemea fedha wanazopokea kupitia vituo hivyo kununua chakula, kulipa karo na pia kupata huduma za afya.
Serikali ya Kenya imesema imefunga vituo hivyo ili kuzuia kundi hilo la Al shabaab kupokea fedha kutoka kwa wafadhili wake katika mataifa ya kigeni.