AF-SOOMAALI

Fidel Castro afariki dunia akiwa na miaka 90


Fidel Castro, kiongozi wa zamani wa Cuba aliyeongoza mapinduzi ya Kikomunisti, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, kakake ametangaza.

“Amiri jeshi mkuu wa mapinduzi ya Cuba alifariki dunia mwendo wa saa 22:29 usiku huu (03:29 GMT Jumamosi),” Rais Raul Castro ametangaza.

Fidel Castro alitawala Cuba kama taifa la chama kimoja kwa karibu miaka 50 kabla ya kakake Raul kuchukua hatamu 2008.

Wafuasi wake walisema alikuwa ameirejesha Cuba kwa wananchi.

Lakini alituhumiwa pia kwa kuwakandamiza wapinzani.

Chini ya uongozi wa Fidel Castro, Cuba ilikuwa na uhusiano maalum na Afrika.

Katika miaka ya 1970 na 80, maelfu ya madaktari na walimu walikwenda Afrika na idadi sawa ya askari wa Cuba walipelekwa huko kuingilia kati migogoro na wakala wa vita baridi hasa nchini Angola.

Akitoa tangazo la kifo cha kakake, Rais Castro, aliyeonekana kuhuzunika sana, aliambia taifa kwenye tangazo la moja kwa moja kupitia runinga usiku kwamba Fidel Castro alikuwa amefariki na mwili wake utachomwa Jumamosi.

Kutakuwa na siku kadha za maombolezo ya kitaifa katika kisiwa hicho.

Raul Castro alihitimisha tangazo lake kwa kutamka kauli mbiu ya mapinduzi ya Cuba: “Twaelekea kwenye ushindi, daima!”

Castro (kushoto) na Che Guevara wakati wa vita vyao dhidi ya serikaliImage copyrightGETTY IMAGES
Image captionCastro (kushoto) na Che Guevara wakati wa vita vyao dhidi ya serikali

Kando na kuandika mara kwa mara gazetini, Fidel Castro alikuwa amestaafu kutoka kwenye siasa kwa muda mrefu, mwandishi wa BBC Will Grant aliyepo Havana anaripoti.

Mwezi Aprili, Fidel Castro alitoa hotuba nadra siku ya mwisho ya mkutano mkuu wa Chama cha Kikomunisti.

Alikiri kwamba alikuwa amezeeka sana lakini akasema maadili ya kikomunisti kwa Cuba bado yana maana na kwamba raia “watashinda”.

“Karibuni nitatimiza miaka 90,” rais huyo wa zamani alisema, na kuongeza kwamba ni “jambo ambalo sikuwahi kulifikiria lingetimia”.

“Hivi karibuni, nitakuwa kama hao wengine wote, “kwetu sote, wakati wetu lazima utafika””, Castro alisema.

Castro alikabidhi madaraka kwa muda kwa kakake mwaka 2006 alipokuwa anaugua maradhi ya utumbo.

Raul Castro alikabidhiwa rasmi madaraka ya urais miaka miwili baadaye.

Fidel Castro, Tarehe muhimu

Fidel Castro (centre) and members of his leftist guerrilla movement in Havana. Photo: January 1959Image copyrightAFP/GETTY IMAGES
  • 1926: Azaliwa mkoa wa kaskazini mashariki wa Oriente nchiniCuba
  • 1953: Afungwa jela baada ya kuongoza maasi ambayo hayakufanikiwa dhidi ya utawala wa Batista
  • 1955: Aachiliwa huru kutoka jela chini ya mkataba wa msamaha
  • 1956: Akiwa na Che Guevara, aanza vita vya kuvizia dhidi ya serikali
  • 1959: Amshinda Batista, na kuapishwa waziri mkuu wa Cuba
  • 1961: Awashinda wapiganaji waliofadhiliwa na CIA waliovamia Bay of Pigs
  • 1962: Atifua mzozo wa makombora wa Cuba kwa kukubali USSR iweke makombora Cuba
  • 1976: Achaguliwa rais na bunge la Cuba
  • 1992: Aafikiana na Marekani kuhusu wakimbizi wa Cuba
  • 2008: Ang’atuka madarakani kwa sababu za kiafya