CULTURE

Jifunze Kiswahili uwafunze na wengine


Kinachosubiriwa ni kuwa na mipango thabiti  ya kukikuza katika medani za ufundishaji shuleni, uandishi  wa vitabu, matumizi yake katika vyombo vya habari kama redio, runinga na magazeti. Tunataka vyuo vya ualimu viwe na walimu waliobobea katika lugha na fasihi ili waweze kuwaandaa walimu wa shule za msingi na sekondari.

 Serikalini nako kuwe na msukumo wa kukitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano kama ilivyokuwa enzi za utawala wa Mzee Rashid Mfaume Kawawa alipotoa agizo la kukienzi Kiswahili kwa kukitumia katika shughuli zote za kikazi. Si hivyo tu ila siku za nyuma wakati wa utawala wa kikoloni hadi baada ya kupata uhuru katika awamu ya kwanza ya uhuru wetu, kulikuwa na agizo la serikali la kufanya mitihani ya Kiswahili katika ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni kufanya mitihani ya Kiswahili chepesi (Lower Kiswahili Examination) kwa wafanyakazi wa madaraja ya chini. Pia kulikuwa na mtihani ya Kiswahili kigumu kwa wafanyakazi wa ngazi ya juu (Higher Kiswahili Examination). Ilikuwa ni lazima kushinda mitihani hii kabla ya kupandishwa daraja. Lengo la mafunzo haya ni kuimarisha matumizi ya Kiswahili serikalini.

Swali la kujiuliza ni je, kwa nini utaratibu huu ulifutwa? Jibu chepesi ni kwamba kasumba imetawala vichwa vya viongozi wa nchi yetu. Kama kweli wanathamini utu wa Mtanzania wasingeacha misingi iliyowekwa na waasisi wa nchi yetu na kuthamini lugha za kigeni ambazo nazo hawazifahamu barabara.